KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Mabingwa watetezi waliogeuzwa vibonde
DOHAR, QATAR. ZIKIWA zimebaki siku 8 kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia kule Qatar, gazeti la Mwanaspoti inakuletea mataifa yaliyowahi kubeba taji hili katika michuano tofauti lakini baada ya miaka minne katika michuano iliyofuata zikageuzwa nyanya wakati zikijaribu kutetea taji lao.
Mataifa haya yaliyofika katika fainali mpya kama mabingwa watetezi lakini yakaishia kukiona chamoto ni pamoja Ufaransa, Brazil, Ujerumani na Hispania.
Je? Ufaransa itaweza kutetea ubingwa wake ilioutwaa mwaka 2018 au itarudia yaleyale yalijitokeza katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Japan/Korea mwaka 2002? Hayo ni maswali ambayo kila mtu anajiuliza huku mashabiki wakisubiri kwa hamu fainali za mwaka huu zitakazofanyika Qatar.
Ujerumani – Kombe la Dunia 2018
Katika fainali hizi za Kombe la Dunia zilizofanyika Russia, Ujerumani ilishindwa kutetea ubingwa wake ilioubeba mwaka 2014 kwenye fainali zilizofanyika Brazil. Katika mechi za kufuzu, Ujerumani ilishinda mechi tisa na kutoa sare mchezo mmoja. Licha ya kufuzu kibabe, Ujerumani ilipata pigo kwani mchezaji wake muhimu kwenye kikosi Marco Reus aliumia katika mechi ya kirafiki siku chache tu kabla ya fainali hizo hazijaanza. Ujerumani ilifanikiwa kubeba ubingwa baada ya ushindi wa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Mario Gotze dhidi ya Argentina na kumfanya Lionel Messi atangaze kustaafu kuchezea timu ya taifa ya Argentina kabla ya kubembelezwa na kurejea.
Baada ya mafanikio hayo, Ujerumani ikafuzu tena kucheza fainali zilizofuata za Kombe la Dunia zilizofanyika Russia 2018. Tena ilifuzu kibabe saba ikishinda mechi zote 10. Lakini ilipoenda katika fainali za 2018 ilifungwa mabao 2-0 dhidi Korea Kusini katika mechi ambayo ilihitaji ushindi ili iende raundi ya 16 bora lakini ikaangukia pua.
Hispania – Kombe la Dunia 2014
Hispania ilishiriki fainali hizi za Kombe la Dunia zilizofanyika Brazil ikiwa bingwa mtetezi baada ya kushinda taji hilo mwaka 2010 katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika kwa mara ya kwanza ndani ya bara la Afrika, kule Afrika Kusini. Hispania iliweka rekodi mbovu katika michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika mwaka 2014 kwani ilimaliza nafasi ya tatu kwenye kundi ikishindwa hata kutinga raundi ya 16 bora. Katika kundi lao Uholanzi na Chile ndio zilizosonga mbele.
Ufaransa – Fainali za Kombe la Dunia 2002
Ufaransa ilibeba Kombe la Dunia katika ardhi yake ya nyumbani mwaka 1998 kabla ya kubeba ndoo ya Euro mwaka 2000. Lakini fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka 2002 Korea na Japan, zilikuwa chungu kwao. Ufaransa ilicheza mechi ya kwanza hatua ya makundi dhidi ya Senegal na Waafrika hao waliwashangaza mabingwa watetezi kwa kipigo cha bao 1-0 lililofungwa na Papa Bouba Diop. Haikuishia hapo Ufaransa ikalazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya Uruguay kabla ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 ilipocheza dhidi ya timu ya Denmark na kuvuliwa ubingwa wao. Ufaransa iliambulia pointi moja tu katika kundi na kuondolewa katika michuano hiyo.
Brazil – Kombe la Dunia 1966
Baada ya kushinda taji la pili la Kombe la Dunia, Brazil ikashiriki tena mwaka 1996 katika fainali nyingine zilizofanyika England baada ya miaka minne. Mabingwa watetezi walianza vizuri kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Bulgaria, mechi iliyofuata Brazil ikapokea kichapo cha maabo 3-1 ilipocheza dhidi ya Hungury kisha ikaondoshwa katika mashindano baada ya kichapo cha 3-1 kutoka kwa Ureno. Brazil ikamaliza kundi katika nafasi ya tatu nyuma ya Ureno na Hungary.
No Comment! Be the first one.