MwaZO wa Ligi Kuu kati ya Geita Gold na KMC umemalizika kwa sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita huku mvua ikitibua burudani kwenye mtanange huo na kusababisha boli lishindwe kutembea.
Mtanange huo umepigwa kuanzia saa 10 jioni ukiambatana na Mvua ambayo ilinyesha muda mfupi kabla ya kuanza mchezo kisha ikarejea kipidi cha pili na kufanya uwanja kuwa na maji ambayo yamesababisha wachezaji kutoonyesha ufundi wao kwani timu hizo zinafahamika kwa soka la chini lenye pasi na ufundi mwingi.
Mabao yote yamefungwa kipindi cha kwanza ambapo wenyeji Geita Gold ndiyo wametangulia kupitia kwa Saido Ntibazonkiza aliyefunga katika dakika ya 36 kwa mkwaju wa faulo ya moja kwa moja huku KMC wakisawazisha mnamo dakika ya 40 kupitia kwa Waziri Junior kwa shuti kali baada ya piga nikupige langoni mwa Geita Gold.
Baada ya kufunga bao hilo, Ntibazonkiza anakuwa amehusika kwenye mabao matano ya Geita Gold kati ya 12 iliyofunga msimu huu, akifunga matatu na kutoa pasi mbili za mabao wakati Waziri Junior likiwa bao lake la kwanza msimu huu na la 41 katika soka la kulipwa.
Kipindi cha kwanza kimekosa ufundi kutokana na hali ya uwanja na timu zote kulazimika kutumia mipira mirefu ambapo wachezaji Masoud Kabaye wa KMC na Juma Mahadhi wa Geita Gold wameonyeshwa kadi za njano.
Kipindi cha pili timu zote zimefanya mabadiliko ya wachezaji ambapo Geita Gold wamewapumzisha Geoffrey Manyac, Offen Chikola, Juma Mahadhi, Arakaza McAthur na Kelvin Nashon na kuingia Juma Luizio, Edmund John, Seleman Ibrahim, Sebusebu Samson na Erick Yema katika dakika ya 46, 64, 74 na 81.
KMC imewapumzisha Baraka Majogoro na Emmanuel Mvuyekule na kuingia Ibrahim Ame na Kenny Ally katika dakika ya 68 na 84.
Kipa wa Geita Gold, Arakaza McAthur na kiungo wa KMC, Baraka Majogoro wameshindwa kuendelea na mchezo huo baada ya kupata majeraha kwa nyakati tofauti uwanjani mnamo dakika ya 68 na 74 nafasi zao zikichukuliwa na Sebusebu Samson na Ibrahim Ame.
Sare hiyo inaifanya KMC kuondoka na pointi moja Kanda ya Ziwa baada ya kucheza mechi mbili ikifungwa moja na sare moja ambapo ilipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Kagera Sugar katika Uwanja wa CCM Krumba, Mwanza.
Geita Gold inaendelea kuiweka salama rekodi yao ya kutopoteza mchezo katika Uwanja wake wa Nyankumbu, ambapo msimu huu huo ni mchezo wa pili uwanjani hapo mchezo wa kwanza ikiwa dhidi ya Namungo ambao walishinda mabao 2-0 huku sare hiyo ikiwa ya tano kwa Wachimba madini hao msimu huu kwenye ligi.
Timu hizo zinafikisha pointi 14 baada ya kucheza michezo 11 na kusalia kwenye nafasi zao, KMC ikikamata nafasi ya tisa na Geita Gold ya 10.
No Comment! Be the first one.